
TUGHE TANGA WATOA MSAADA HOSPITALI YA AFYA YA AKILI LUTINDI KOROGWE
2025-03-07
Katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) Mkoa wa Tanga walitembelea na kutoa msaada wa mahitaji mbalimbali kwa wagonjwa wenye Afya ya akili katika Kliniki ya Afya ya akili Lutindi(Lutindi Mental Clinic) iliyopo Wilayani Korogwe. Msaada uliotolewa katika ziara hiyo ni pamoja na magodoro, vyombo, jora la vitambaa kwa ajili ya sare, sukari, mchele, taulo za kike pamoja na vitenge kwa ajili ya wagonjwa hao. Akizungumza mara baada ya kukabidhi misaada hiyo Mwenyekiti wa Tughe Mkoa wa Tanga Best Jerry Mitondwa alisema kuwa huo ni utaratibu wao ambao wamejiwekea kuyafikia makundi mbalimbali yenye uhitaji kwa kuwafariji. Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Katyetye Marwa alieleza kuwa hospitali inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo baadhi ya Wagonjwa kutelekezwa na ndugu zao hasa kipindi wanapokuwa wakiwapeleka kushindwa kuwafuatilia na hivyo kuwa mzigo kwa hospitali kuchukua jukumu la kuwatunza jambo ambalo limekuwa ni changamoto kubwa kwao na kuhitimisha kwa kuwashukuru TUGHE kwa msaada huo ambao utasaidia kwa kiasi kikubwa utolewaji wa huduma hospitalini hapo