TUGHE MKOA WA SHINYANGA WAKABIDHI VIFAA TIBA NA KUCHANGIA HARAMBEE
2026-03-12
Na Mwandishi wetu Shinyanga, Katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kwa mwaka huu, Kamati ya Wanawake TUGHE Mkoa wa Shinyanga kwa kushirikiana na Uongozi wa TUGHE Mkoa walikabidhi msaada wa vifaa tiba katika Hospitali ya Wilaya ya Shinyanga ili kurahisisha utoaji wa huduma za Afya katika Hospitali hiyo. Msaada huo ulikabidhiwa mbele ya Mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa huo Bi. Mboni Mohamed Mhita kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Shinyanga Dkt Kalekwa Kasanga wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambapo yalifanyika katika Kata ya Uyogo Halmashauri ya Ushetu Mkoani Shinyanga. Vifaa vilivyotolewa katika Hospitali hyo ni pamoja na kipima mtiririko wa Oksijeni(Flow Meter), kipima kiwango cha Oksijeni kwenye Damu( Pulse Oximeter), mashine ya kupima sukari kwenye Damu( Glucometer) 2, Mashine ya kudijitali ya kupimia shinikizi la Damu 2, kifaa cha kusikiliza mapigo ya moyo na mapafu (Stetoskopu), mashine ya kupima uzito pamoja na mtungi wa gesi ya kupumulia. Mara baada ya makabidhiano hayo, Dkt . Kalekwa aliishukuru Kamati ya Wanawake TUGHE Mkoa kwa namna walivyoweza kuigusa jamii kwa kuwapatia vifaa tiba vitakavyokwenda kusaidia wagonjwa waliopo katika Halmasha yake. Sambamba na hilo, Kamati ya Wanawake TUGHE wakiongozwa na Mwenyekiti wao Cde . Experentia Misalaba pamoja na Katibu wake Cde . Catherine Masalu walishiriki na kuchangia harambee ya Shule ya Msingi Bukwimba iliyopo Kata ya Uyogo Halmashauri ya Ushetu, ambapo Mkuu wa Mkoa huo aliipongeza na kuishukuru Kamati hiyo na kuwataka waendelee kutatua changamoto mbalimbali katika Jamii kwa kufanya matendo ya huruma