TUGHE YAJIDHATITI KUBORESHA MASLAHI YA WATUMISHI WAKE, YASAINI MKATABA WA HALI BORA NA TAWI LA TUGHE MAKAO MAKUU
2026-01-30
Na Mwandishi Wetu, Morogoro Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) kimedhihirisha dhamira yake ya kuendelea kuboresha maslahi ya Watumishi wake kwa vitendo ambapo siku ya leo Ijumaa tarehe 30/01/2026, Menejimenti na Tawi la TUGHE Makao Makuu wamesaini Mkataba wa Hali Bora (Collective Bargaining Agreement). Mkataba wa Hali bora ambao utakuwa wa kipindi cha miaka miwili umesainiwa leo Mkoani Morogoro na Katibu Mkuu wa TUGHE Cde. Hery Mkunda kwa niaba ya Menejimenti ambaye aliambatana na Mkuu wa Idara ya Sheria TUGHE, Wakili Mwanaidi Mgowa huku Tawi likiwakilishwa na Mwenyekiti wa Tawi la TUGHE Makao Makuu Cde. Cleophace Butahe pamoja na Katibu wa Tawi Wakili Jack Peter Nyaganilwa. Baadhi ya vipengele vilivyoboreshwa katika Mkataba huu wa Hali Bora ni pamoja na kile cha Likizo mbalimbali zinazotambulika kwa mujibu wa Sheria, matibabu ya Watumishi na Wategemezi wao Tuzo kwa Wafanyakazi Hodari, malipo ya kiinua mgongo (gratuity) na Malipo ya Leseni za Bodi za Mawakili na Uhasibu. Akizungumza mara baada ya kusaini mkataba huo, Katibu Mkuu wa TUGHE ameupongeza Uongozi wa Tawi kwa kushiriki kikamilifu katika hatua za zote za kuandaa mkataba huo kwa kuleta hoja za maslahi watumishi ambazo zimesaidia kuboresha Mkataba wa Hali Bora ambao utatekelezwa katika kipindi cha mwaka 2026/2028. Nao viongozi wa Tawi wameishukuru menejimenti kwa kuendelea kufungua milango ya majadiliano na Tawi na kutoa fursa ya kuwasemea watumishi wenzao jambo linalosaidia kupata ufumbuzi wa haraka kunapotokea changamoto za masuala mbalimbali ya watumishi wa TUGHE. Mkataba huu utawahusu Wafanyakazi wote walio katika Ajira ya kudumu na Ajira za Mikataba muda Maalumu na Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE).